Mgombea wa ugavana kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir anatarajiwa kuongoza zoezi la ufunguzi wa shule ya upili ya Wasichana ya Mekatilili siku ya Jumamosi.

Akizungumza kwenye kongamano lililojumuisha jamii ya Mijikenda, Nassir amesema shule hiyo yenye maabara ya kisasa na iliyojengwa kupitia ufadhili wa pesa za ustawi wa eneo bunge la Mvita NG-CDF imejengwa kama njia moja wapo ya kuthamini na kuhifadhi historia za aliyekuwa mwanamke jasiri na shujaa nchini Mekatili Wa Menza.

Kulingana na Nassir shule hiyo ambayo imejengwa eneo bunge la Mvita ni miongoni mwa shule kubwa Zaidi za wasichana zilizojengwa ukanda wa pwani.

Wakati huo huo Nassir anatarajiwa kufungua uwanja wa kisasa wa michezo wa Ronald Ngala Stadium siku ya jumapili katika shule ya msingi ya Ronald Ngala hapa jijini Mombasa.

Kulingana na Nassir uwanja huo wa kisasa utakuwa ni wenye kuandaliwa michuano mbalimbali kama njia moja wapo ya kuinua sekta ya michezo kaunti ya Mombasa na pwani kwa ujumla.