Waziri wa elimu profesa George Magoha, ameonya walimu wakuu dhidi ya kuwafukuza wanafunzi kuendea karo wakati huu.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua madarasa ya mtaala mpya wa elimu wa CBC katika shule ya upili ya Rev. Gitau na ile ya wavulana ya Alliance huko Kikuyu kaunti ya Kiambu, Profesa Magoha amesema haifai kuwatuma wanafunzi nyumbani ilhali watakwenda likizo fupi tarehe tisa mwezi Agosti, ili kutoa fursa ya kuandaliwa kwa uchaguzi.

Ametoa wito kwa walimu wakuu wawaite wanafunzi walio nyumbani ili waweze kufanya mitihani ya katikati ya muhula.

Amesema walimu hao wakuu wanaweza kuzungumza na wazazi walipe karo katika kipindi hicho cha likizo kabla ya masomo kurejelewa Agosti 11.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kutatiza kalenda ya masomo kwani shule kadhaa zitatumiwa kama vituo vya kuhesabia kura.

Kulingana na taarifa ya tume huru ya uchaguzi na mipaka, takriban shule 250 kote nchini zitatumiwa kama vituo vya kuhesabia kura.