Rais William Ruto ameagiza Mamlaka ya Kusimamia Polisi (IPOA) kuipa Wizara ya Mambo ya Ndani mkakati wa kina wa jinsi ya kukomesha mauaji ya kiholela nchini.


Akiongea katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na IPOA kujadili wajibu wao, Ruto amesema serikali yake imejitolea kuondoa uhalifu huo kikamilifu.

Maagizo yake yanakuja katika muktadha wa agizo lingine alilotoa wiki mbili zilizopita, ambapo aliamuru kwamba uchunguzi uanze kuhusu matukio ambapo maafisa wa polisi wameshutumiwa kwa mauaji yasiyo ya kisheria.

IPOA hata hivyo iliibua mashaka na uchunguzi huo, ikitaka Kitengo cha Masuala ya Ndani cha Huduma ya Polisi ya Kitaifa kusitisha uchunguzi wa madai ya mauaji ya kiholela yaliyofanywa na Kitengo cha Huduma Maalumu (SSU) ambacho sasa kimevunjwa.

Mwanachama wa bodi ya IPOA John Waiganjo Jumatatu iliyopita alisema uchunguzi unapaswa kuachiwa mamlaka ya uangalizi, akisema kuwa huduma ya polisi haiwezi kujichunguza yenyewe.

DCI ilitangaza kuvunjwa kwa SSU kupitia taarifa mnamo Oktoba 16, ikitaja amri hio kutoka kwa kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Noor Gabow.