Ipo haja ya vijana kuhusishwa kikamilifu katika masuala ya kupambana na visa vya dhulma vya kijinsia katika kaunti ya Kwale.

Hii ni kulingana na Dina Otieno kutoka shirika la sauti ya wanawake pwani.

Akizungumza katika kikao cha uhamasisho wa masuala ya kupambana na visa vya dhulma za kijinsia kilichoandaliwa na shirika la Equality Now kwa kuwajumuisha vijana katika kaunti hiyo Dina ameweka wazi kuwa vijana wamekuwa wakitengwa katika harakati za kupambana na kukomesha dhulma katika jamii.

Vile vile ameihimiza serikali ya kaunti hiyo kushirikiana kwa ukaribu na mashirika mbalimbali kukomesha dhulma kwani visa hivyo vinazidi kuongezeka licha ya juhudi zinazoendelzwa.

Kwa upande wake Mbarak Mwamaku aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya vijana amesema ukosefu wa elimu ya kupambana ni dhulma umechangia pakubwa visa hivyo kuongezeka na kukosa kusuluhishwa.

Kauli yake imeungwa mkono na Zaliha Mohamed kutoka Vanga, ameongeza kuwa ukosefu wa ajira uliosababishwa na janga corona imechangia kuongezeka kwa visa vya dhulma katika jamii baada ya wengi kupoteza ajira zao.