Huenda maazimio ya serikali ya kuimarisha sekta ya uchumi wa bahari kupitia Blue economy ukaathirika pakubwa kutokana na uchafuzi wa bahari unaotoka na uchafu wa plastiki.

Kulingana na Nancy Githaiga kutoka shirika la ufadhili wa mazingira WWF amebainisha kuwa asilimia 80 ya plastiki zinazotumika huishia katika maziwa na baharini na kusababisha kupungua kwa idadi ya samaki.

Katika mkao wa kutafuta mwafaka wa uhifadhi wa mazingira ya bahari ulioandaliwa na shirika hilo la WWF, Githaiga vile vile ameeleza kuwa plastiki hizo mwishowe huathiri afya ya binadamu kutokana na kula samaki ambao hula plastiki hizo zinazotupwa baharini.

Githaiga amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira hususan yale ya bahari.

Vile vile imebainika kwamba taifa la Kenya hukusanya tani nusu milioni ya taka kila siku tani 900 zikitoka kaunti ya Mombasa.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Coastal Marine and Development Mombasa Innocent Wanyonyi amesema kwamba taka hizo ambazo zimezagaa katika maeneo mbalimbali hutoa kemikali zilizo na athari kwa afya za binaadamu.