Vijana wamelaumiwa kwa madai ya kuwa waoga na kutoonesha nia ya kuwania nyadhifa tofauti za kisiasa hapa Mombasa.

Kulingana na Mwanaharakati Brian Osiema ambae pia ni mwanasiasa kaunti ya Mombasa, idadi ya vijana humu nchini ni takriban asilimia 60 na kwamba wanafaa kupewa kipaumbele katika masuala ya uongozi.

Aidha Osiema amewalaumu vijana kwa kutowaunga vijana wenzao wakati wa kuwania nyadhifa za kisiasa na badala yake kuwachagua watu wengine.

Osiema amewasihi vijana kujitokeza kwa wingi na kusajiliwa kama wapiga kura na pindi wakati wa uchaguzi unapofika wawachague viongozi ambao ni vijana na wenye maono ya maendeleo.

Amesema iwapo hayo yatazingatiwa, basi sauti ya vijana itaheshimika popote na vilio vyao kuzingatiwa ipasavyo.