Familia 3 kutoka Kisauni kaunti ya Mombasa zimeiomba serikali kubaini walipo jamaa wao watatu baada kutoweka kwao katika hali tata siku 19 kufikia sasa.

Watatu hao ni Hussein Mohammed, Fahmi Bakari na Masuo Bakari ambapo wanadaiwa kupotea tarehe 5 Disemba.

Kulingana na Mohammed Hussein Mohammed ambaye ni babake Hussein Mohammed kijana wake anajihusisha na biashara ya matatu na kwamba yeye wenzake walikuwa safarini kutoka Thika kununua matatu amabpo hawakufika Mombasa na baadae gari lao kupatikana eneo la Maungu katika barabara kuu ya kutoka Mombasa kuelekea jiji la Nairobi.

Mohammed amesema kuwa alishangaa kuona gari la mwanawe likiwa salama na mizigo yote kama walivyokuwa wamewasiliana kwenye simu mawasiliano ya mwisho.

Aidha dadake Masuo Bakari, Halima Bakari amesema kutoweka kwa ndugu yao kumewaweka katika hali ngumu ikizingatiwa kuwa yeye ndiye alikuwa ndiye alikuwa tegemeo katika familia.

Kwa pande wake Fatuma Bakari Shekuwe dadake Fahmi Bakari amekana madai yoyote ya kakake kuhusishwa na magenge ya kihalifu au uhalifu wa aina yoyote na kwamba siku 19 tangu kupotea kwao hawajapata taarifa zozote kuwahusu wakiitaka idara ya usalama kuwafichua waliko.

Afisa wa masuala ya dharura katika shirika la kutetea haki za kibinadamu la MUHURI Francis Auma Mbela amesema licha ya mashirika hayo kuzungumzia visa hivyo, vimezidi kutokea na sasa wanaitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuvichunguza visa hivyo ili wakenya wanaowapoteza jamaa wao wapate haki pamoja na kukomesha visa vya watu kupotezwa kiholela.