Jamii ya watu wenye ulemavu katika kaunti ya Mombasa wanaendelea kulalamikia kutengwa katika mambo tofauti ikiwemo umiliki wa rasilimali.

Wakiongozwa na Lucy Chesi kutoka shirika la kutetea haki watu wenye walemavu la Tunaweza Women with Disability Group amesema kuwa jamii hiyo imetengwa hasa katika umiliki wa rasilimali ikiwemo ardhi.

Amesema hali hiyo imesababisha jamii hiyo kusalia nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na watu wengine.

Aidha mwanaharakati huyo amesema ipo haja ya serikali kuwekeza katika elimu ya watu wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira mwafaka akitaja kuwa shule nyingi humu nchini haziangazii jamii hiyo na kupelekea wao kusalia nyuma kielimu.

Wakati uo huo amelikosoa baraza la kusimamia maslahi ya walemavu “National Council of People with Disability” nchini kwa kile anachokidai kuwa limeshindwa kuhudumia jamii hiyo ipasavyo.