Kenya imetajwa kuwa haijapiga hatua zozote katika kuangazia maslahi na haki za kibinadamu.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika Salma Hemed amesema licha ya mashirika ya kijamii kufanya juhudi katika kuliangazia suala hilo, bado Serikali ya kitaifa imekuwa kikwazo kikuu katika vita dhidi ya dhuluma za kibinadamu.

Salma amesema visa vya mauaji ya kiholela na watu kupotezwa limechangia madhila mengi mno katika familia zinazoathirika na matukio hayo.

Wakati uo huo, afisa huyo ameitaka jamii hasa ya eneo la Pwani kutosalia kimya bali kupigania haki zao ili kudhibiti dhuluma nyingi wanazotendewa na hasa vitengo vya usalama.