Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika mtaala mpya wa elimu licha ya kuwepo kwa pingamizi kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu mtaala huo.

Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, waziri wa elimu Profesa George Magoha amesema mtaala huo unaendelea vyema na kwamba serikali itaendelea kuwekeza fedha zaidi na kupuuzilia mbali madai ya baadhi ya watu kuwa unaoneloea kufeli tangu kuzinduliwa na serikali.

Magoha amesema licha ya kuwepo kwa kesi mahakamani ya kuupinga mtaala huo, serikali itaendelea kuekeza pesa zaidi ili kuufanikisha ikiwemo ujenzi wa madarasa elfu 10 mapya mradi uliyozinduliwa na rais Uhuru Kenyatta ili kukidhi uhaba wa madarasa nchini chini ya mtaala mpya.

Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa madarasa 5,200 unaendelea na kwamba unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka ujao huku mradi wote wa darasa elfu 10 ukitarajiwa kukamilika kufikia mwaka 2023.

Waziri huyo aidha amesema tangu mwaka wa 2018, serikali imeweza kutumia shilingi bilioni 28.5 kwa kununua vitabu kwa wanafunzi wa shule za msingi pamoja na shule za upili.

Magoha ameongeza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa watoto wote wanaenda shuleni kwa kufanya masomo ya shule za msingi kuwa bure na kupunguza karo ya shule za upili na hivyo ni sharti kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni.
Wakati uo huo amewaonya wakuu wa shule dhidi ya kuwatoza ada za ziada wanafunzi.

Magoha ameyasema haya baada ya kuzindua ujenzi wa madarasa mawili ya kufanikisha mtaala wa CBC katika shule ya upili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum huko Bombolulu na baadae kukagua ujenzi unaoendelea wa shule ya upili ya wasichana ya Mama Ngina huko Shanzu.