Kinyang’anyiro cha useneta katika kaunti ya Kilifi kinaendelea kupamba moto baada ya afisa mkuu wa wizara ya mipangilio ya uchumi katika kaunti ya Kilifi kuacha kazi na kujitosa kwenye siasa rasmi.

Ben Kai amesema kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kushauriwa na wananchi wa Kilifi kuwania kiti hicho cha useneta ili kuleta mabadiliko ya uongozi na kuwahudumia wananchi vyema.

Kai anatarajiwa kupambana na seneta aliyeko mamlakani kwa sasa Stewart Madzayo ambaye anatetea kiti chake kwa chama cha ODM.

Amebaini kuwa atawania kiti hicho kupitia chama cha Pamoja African Alliance yaani PAA.

Hatua yake inajiri huku maafisa wengine wa kaunti ya Kilifi wanaowania viti mbalimbali vya kisiasa wakiwa wameacha kazi.