Wagombea wa nyadhifa mbalimbali za uongozi kupitia chama cha ODM kaunti ya Mombasa wamehimizwa kufanya maandalizi bora wanapoelekea katika kura za mchujo ili kuepuka vurugu kutokea wakati wa zoezi hilo katika chama hicho.

Akizungumza na wagombeaji wa viti vya uwakilishi wadi katika kaunti ya Mombasa kupitia kwa chama cha ODM, muwaniaji kiti cha ugavana kupitia kwa chama hicho Suleiman Shahbal amewataka wagombea hao kujitayarisha ipasavyo kabla ya zoezi hilo la mchujo kuandaliwa. 

Amewataka wagombea hao kuhakikisha kuwa wameweza kusajili wanachama wengi ambao watakuwa na uhakika kwamba watawaunga mkono.

Shahbal aidha amemtaka mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Mombasa Mohammed Hamid Khamis kuwahusisha vilivyo wagombea wote wa viti mbalimbali katika kaunti hiyo katika matayarisho ya kura za mchujo za chama hicho ili kuhakikisha kuna uwazi na usawa kwa wagombea wote wa chama hicho.

Wakati uo huo, Shahbal amewaonya vikali wanasiasa wanaolenga kutumia vyeti ghushi katika harakati za kuwania nyadhifa mbalimbali za uongozi akiitaka tume ya IEBC kuvichunguza kwa makini vyeti vyotre vitakavyowasilishwa na wawaniaji mbalimbali.