Mjane mmoja katika eneo bunge la Nyali Kaunti ya Mombasa analilia haki kwa madai ya kunyang’anywa nyumba aliyowachiwa na mumewe.

Mjane huyo anadai mwekezaji mmoja wa kibinafsi amemfurusha kutoka kwa nyumba hio.

Emmy Andisi Agango, mama wa watoto 6 na anayeishi katika mtaa wa Rainbow Estate, Nyali amesema alifurushwa katika jumba hilo alilowachiwa na mumewe Nahashon Juma Agango aliyeaga dunia mwana wa 2007.

Amesema kutokana na hali hiyo amelazimika kuishi barabarani na wanawe bila ya msaada wowote.

Akizungumza na Wanahabari nje ya jumba hilo, Agango amesema juhudi zake za kutafuta haki katika afsisi za ardhi Kaunti ya Mombasa hazikufua dafu.

Afisa wa maswala ya kisheria kutoka Shirika la Kenya Legal Defence Fund Martin Oduogi amesema vibali vyote alivyotumia Abdelhamed Ahmed Alhassan kumnyang’anya mama huyo jumba hilo ni ghushi.

Stakabadhi hizo zinadaiwa kutolewa na mahakama kuu Mjini Mombasa.

Mwandishi:Ibrahim Mudibo