Baraza la wazee wa chonyi kaunti ya Kilifi limemuidhinisha Ben Kai kuwania rasmi kiti cha usineta katika kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu jao.

 

 Hafla hiyo ambayo imefanyika katika eneo la Chonyi  na kuhudhuriwa na  viongozi kutoka kwa mbari zote za jamii hiyo, imekuwa kigezo kikuu kwa siasa za Kai huku akiahidi kuleta maendeleo pindi tu atakapochaguliwa kuwa seneta wa kilifi.

 

Mwenyekiti wa baraza hilo Kenga Lewa amewataka wakazi wote wa kaunti hiyo kumuunga mkono Ben Kai kwenye kinyanganyiro hicho kwani atapambana na seneta aliyemamlakani kwa sasa Stewart Madzayo.

 

Kulingana na Lewa kaunti ya Kilifi inahitaji seneta ambaye ataimarisha maendeleo na kukabiliana na masaibu ambayo yanawakumba wakazi wa Kilifi.

 

Kwa Upande wake Kai amesema kuwa yuko na tajriba ya uongozi kwani ameendeleza miradi ya kimaendeleo wakati alipokuwa afisa mkuu wa wizara ya fedha katika kaunti hiyo.

 

Mwenyekiti wa wasomi katika eneo hilo la Chonyi Dr.Titus Tunje Kadere ameitaka jamii hiyo kuwa na ushirikiano mkubwa kwenye uchaguzi wa agosti mwaka huu.