Wavuvi kwenye ufuo wa bahari wa Nyali wamelalamikia mradi wa nyaya za mawasilano ambao umeanza kutekelezwa kupitia kwa ufuo huo na kampuni ya mawasiliano nchini ya Telkom Kenya.

Wakiongozwa na Said Abdulrahman wavuvi hao wanasema kuwa hawajahusishwa katika mradi huo na kutaka mradi huo kusitishwa hadi pale washikadau wa mradi huo watakapofanya mazungumzo nao.

Abdulrahman amesema kuwa kabla ya mradi huo kuendelea ni sharti kwa wadau wote wanaohusika kushirikishwa ili kupatikana kwa suluhu mwafaka ikiwemo kufidiwa kutokana na athari zake iwapo utaendelea.

Aidha wavuvi hao wamedai kulaghaiwa na wasimamizi wa mradi huo kwa muda mrefu hali ambayo wamesema inazidi kuwakera.

Wakati uo huo, mwanaharakati wa masuala ya ardhi na ambaye pia ni wakili katika shirika la kutetea haki za binadamu la HAKI YETU Munira Ali amesema hata baada ya makubaliano ya kampuni hiyo na waathiriwa hao ya kulipwa fidia kutiwa saini, kampuni hiyo imekiuka makubaliano hayo akiitaka serikali kuingilia kati suala hilo.