Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya ugonjwa wa kifua kikuu yani TB, Jumuiya ya mataifa wanachama wa IGAD afrika inapambana kutokomeza ugonjwa huo.

Licha ya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayolemewa na makali ya ugonjwa wa kifua kikuu, IGAD kupitia msimamizi wake daktari Fatma Adan amesema wanashirikiana na wanachama wa mataifa ya IGAD kuhakikisha wanaboresha huduma za kutibu kifua kikuu.

Adan amesema nchi nyingi zinazopakana na Kenya zinalemewa na ugonjwa huo na kuwapelekea kutafuta huduma za matibabu katika taifa hili la Kenya.

Ameongeza kuwa jamii za wanaohama kutoka taifa moja hadi jingine ni miongoni mwa wanaosumbuliwa na magonjwa kama kifua kikuu huku akieleza kuwa ukosefu wa huduma bora za afya mipakani inachangia ongezeko la magonjwa yanayoambukizwa.

Kwa upande wake afisa wa afya katika wizara ya afya nchini Joseph Sietenei amesema ugonjwa huo wa kifua kikuu ni ugonjwa unaoambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia hewa.

Aidha ametoa wito kwa umma kupima ugonjwa wa kifua kikuu mara kwa mara ili kuanza matibabu yanayotolewa bure na serikali endapo mtu atapatikana na ugonjwa huo.

Vilevile amehimiza wagonjwa wa kifua kikuu kuhakikisha kuwa wanamaliza dozi ya dawa kulingana na walivyoagizwa na daktari huku akisema kuwa wagonjwa wasiomaliza dozi huathirika sana na ugonjwa huo baadaye.