Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria amekashifu na kulaani kisa cha kushambuliwa kwa wanahabari katika makao makuu ya Chungwa House ,akitaja kuwa hio ni ishara tosha ya uongozi mbaya utakaoletwa na kinara wa ODM Raila Odinga.

Kupitia ujumbe aliochapisha katika ukurasa wa Facebook, Kuria amesema kwamba hata mgombea mwenza wa Odinga anaweza kushambuliwa na asichukue hatua yoyote.

Kauli ya Kuria ilijiri baada ya wanahabari wawili kushambuliwa na kundi la watu katika mkutano wa kinara wa Azimio Raila Odinga huko Chungwa House.

Mwanahabari wa Standard, Moses Nyamori alishambuliwa na walinzi wa Chungwa House kwa kile kinachosemekana kuwa aliandika makala ambayo yaliwagusa viongozi wakuu katika chama cha ODM.

Walinzi hao ambao walikuwa wakipokea amri kutoka kwa mkubwa wao, Benard Kadundo walimshambulia mwanahabari huyo na kumtupa nje ya makao ya ofisi hiyo, ambapo Raila Odinga alikuwa anampokea gavana Joseph Ole Lenku ambaye aligura chama cha Jubilee.

Kwingine ripota wa gazeti la Star, Luke Awich pia alishambuliwa na simu yake kuharibiwa.ODM baadaye waliomba msamaha kwa vyombo vyote vya habari na kuahidi kutorudiwa kwa kisa kama hicho tena.