Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir ameahidi kuboresha uchumi kwa manufaa ya jamii za kaunti ya Mombasa pindi atakapo chukuwa hatamu ya uongozi wa serikali ya kaunti ya Mombasa baada ya Agosti 9.

Akizungumza katika hafla iliyoileta pamoja jamii ya Mulembe katika uwanja wa shule ya chekechea ya Kwahola eneo la Changamwe Nassir amesema kuwa janga la virusi vya Corona liliathiri pakubwa uchumi.

Aidha Nassir ambaye anagombea kiti cha ugavana ,amedokeza kuwa katika manifesto yake aliyoyapa kipao mbele ni kuhakikisha kuwa uchumi wa kaunti ya Mombasa unaimarika.

Wakati huo huo Nassir ameahidi kuwapunguzia ada wanazotozwa wafanyibiashara wadogo wadogo pindi tu atakapo chukuwa hatamu ya uongozi wa serikali ya kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Nassir ni kuwa kwa muda mrefu wafanyibiashara wadogo katika maeneo mbali mbali hapa Mombasa wamekuwa wakilalamikia suala la ada katika biashara zao.

Kadhalka Nassir amewaomba wafuasi wa ODM kuwa na msimamo na kuepuka kubadili chama.Kwa upande wake mbunge wa Jomvu Badi Twalib amemtaja muaniaji ugavana kaunti ya Mombasa Abdulswamad Nassir kama kiongozi atakayeleta maendeleo katika eneo hilo.

Kwa upande wake Abdulswamad Nassir amewataka wakaazi wa eneo bunge la Jomvu kumchagua tena badi kutokana na kazi aliyowafanyia.