Harakati za utetezi wa kijamii na upiganiaji wa haki za kibinadamu zimetajwa kudorora kwa kiwango kikubwa katika kaunti ya Lamu.

Mwanaharakati wa kijamii kaunti ya Lamu na ambaye anajihusisha na ufuatiliaji wa maswala ya bajeti Jafari Masoud amesema wanaharakati wengi wa kijamii katika kaunti ya Lamu wamelemaa licha ya kuwa changamoto za kijamii bado ziko.

Amesema baadhi ya wanaharakiti wa kijamii wameacha kazi zao za uwanaharakati baada ya kuajiriwa na serikali ya kaunti jambo ambalo limefanya baadhi yao kuwa vibaraka wa viongozi wa kisiasa.

Masoud ameongeza kuwa baadhi yao wameacha kazi ya uwanaharakati kwa kuolewa na waume ambao kanuni zao haziendeni na kazi hiyo ambapo hawapewi ruhusa ya kujumuika na wenzao katika kazi za utetezi wa umma.

Ametoa wito kwa watetezi wa haki za kibanadamu kaunti ya Lamu kuendelea na kazi zao za utetezi wa umma hata kama mtu ameandikwa kazi na serikali.

Amewataka wanaharakati wa kijamii walioajiriwa na serikali kutumia fursa hiyo kuwatetea wananchi kikamilifu ikizingatiwa kuwa wako karibu zaidi na viongozi na wako na nafasi kubwa ya kusikizwa.