Huduma za mawasiliano ya mtandao nchini zinatarajiwa kuimarika zaidi baada ya kampuni ya mawasiliano ya Telkom Kenya kupokea nyuzi  za mawasiliano katika ufuo wa Nyali.

Trizer Odero na taarifa zaidi

Nyuzi hizo kwa jina Pakistan & East Africa Connecting Europe (PEACE CABLE) ni ya kibinafsi na ya sita humu nchini na bara la Afrika Mashariki, ikitokea taifa la China ambayo imegharimu Dola millioni 400.

Waziri wa mawasiliano, teknolojia na masuala ya vijana nchini Joe Mucheru amesema kuwa nyuzi hizo ni za muhimu katika mawasiliano ya kila siku ikizingatiwa kwamba kwa sasa watu wengi nchini wanatumia mtandao.

Kauli yake imeungwa mkono na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Telkom Kenya Mugo Kibati akiongeza kwamba nyuzi hizo zitaimarisha na kuboresha  mawasiliano baina ya Kenya, jumuiya ya Afrika Mashariki na dunia nzima.

Akigusia kuhusu malalamishi yaliyoibuliwa na baadhi ya wavuvi wa fuo hiyo kwamba nyuzi hizo zitaathiri shughuli za uvuvi, Kibati amepuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa zimepita chini ya bahari na kamwe hazina athari yoyote.

Aidha waziri Mucheru, ametaka siasa kutoingizwa kwenye mradi huo na badala yake kuzingatia umuhimu wake katika sekta mbalimbali hasa sekta za kibiashara.

Kwa upande wake waziri mawasiliano, teknolojia kaunti ya Mombasa Anwar Ahmed amesema nyuzi hizo zitawezesha kutimia kwa ruwaza ya kaunti ya Mombasa kuwa katika nafasi nzuri ya kuboresha biashara za mitandaoni.

Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo