Baadhi ya viongozi wa ODM hapa Mombasa wanaendeleza kampeni za Azimio la Umoja kumpigia debe kinara wa chama hicho Raila Odinga kuwa rais wa 5 wa Jamhuri ya Taifa la Kenya.

Wakipeleka kampeni hizo eneo bunge la Likoni viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir,Mishi Mboko wa Likoni na mwenzao wa Jomvu Badi Twalib wamedokeza kuwa Odinga ataleta mabadiliko ya uchumi kwa taifa la Kenya.

Watatu hao aidha wameeneza sera na Agenda za Odinga kwa wakaazi wa eneo hilo na kuwaomba kumpigia kura kama rais ifikapo Agosti 9.

Wakati huo huo watatu hao wamelaani vikali tukio alilofanyiwa kinara wao Raila Odinga huko Iten kaunti ya Uasin Gishu na kuitaka idara ya usalama kufanya uchunguzi kubaini ni yupi aliyewatuma vijana hao kuweza kurusha mawe kutaka kumuua Odinga.

Kulingana nao tukio hilo ilikuwa ni njama ya wapinzani kutaka kuharibu umaarufu wa Odinga,wakisema kuwa hakuna ghasia zozote zitakazoua azma ya Odinga kuwa rais wa 5 wa Jamhuri ya taifa la Kenya.

Haya yanajiri huku naibu wa rais William Ruto akimuomba msamaha Odinga kuhusiana na tukio hilo.