Gavana wa kaunti ya Taita Taveta Granton samboja amewahakikishia wananchi wanaoendesha shughuli zao kwenye shamba la Machungwani kaunti ndogo ya Taveta ambalo linazozaniwa, kuwa hakuna mwananchi atafurushwa.

Akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa eneo hilo wadi ya Mboghoni, Samboja amesema kuwa serikali itawapa shamba hilo waendeleze shughuli zao za ukulima na pia kujenga makaazi yao maeneo hayo.

Gavana Samboja ameongeza kuwa tayari serikali yake imeanzisha mchakato na serikali ya kitaifa kupitia tume ya kitaifa ya ardhi kuona kuwa wananchi wanaoishi eneo hilo wamekabidhiwa stakabadhi rasmi za umiliki ardhi.

Wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiishi kwa hofu ya kufurushwa baada ya kuzuka tetesi kuwa muda wa umiliki wa shamba hilo umeongezwa.