Migogoro inaendelea kushuhudiwa katika chama cha ODM kaunti ya Kilifi baada ya tetesi kuwa chama hicho hakitaendeleza uchaguzi wa mchujo na badala yake wagombea viti wafanye mazungumzo na kuelewana.

Kwa sasa mirengo tofautitofauti ya kisiasa hasa kwenye uongozi wa ugavana inaendelea kutofautiana vikali huku wafuasi wa chama hicho wakihofia mgawanyiko mkubwa.

Jimmy Kahindi ambaye anaenda mchujo na Gedion Mungaro anasisitiza kuwepo kwa uchaguzi wa mchujo kwa kile alichodai kuwa amekuwa akiuza sera za chama cha ODM mashindani ikilinganishwa na mwenzake Gedion Mungaro.

Kulingana na Jimmy anahofia kuwa tiketi huenda ikapewa Mungaro jambo ambalo amesema kuwa hatakubali kwani itaathiri sana chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Naye mwenyekiti wa chama hicho kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire amewataka wagombea waendeleze mazungumzo na kuelewana ili Kilifi isiwe na uchaguzi wa mchujo.

Hii leo,chama hicho kimeita mkutano wa dharura na viongozi wote wa ODM kaunti ya Kilifi ili kutatua mizozo hiyo.