Hali tata ya usalama katika Gatuzi dogo la Likoni kwa kiwango kikubwa imetajwa kuchangiwa na hali ya vijana wadogo kuzama katika uraibu wa dawa za kulevya katika eneo Likoni.

Chifu wa Likoni Said Juma Kandi amesema ni sharti jamii yenyewe ya eneo hilo ikubali kwamba swala la uraibu wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana wadogo lingali changamoto kubwa.

Kandi ameisihi jamii hiyo kuibuka na mbinu mbadala za kuidhibiti hali hiyo ya matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana wadogo.

Akizungumza na mwanahabari wetu huko Likoni, Kandi amesema ni lazima wazazi wabadili malezi ya Watoto wao na kila mara kuifuatilia mienendo ya wana wao ili kuwaelekeza katika njia njema.

Wakati uo huo, amesisitiza kwamba bila ya wazazi kutekeleza majukumu yao ya ulezi ipasavyo, kizazi kichanga cha eneo hilo la Likoni kitaangamizwa na dawa za kulevya na uhalifu.

Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo