Waziri wa usalama wa ndani daktari Fred Matiang'i amewataka maafisa wa utawala kote nchini kuhakikisha kwamba usalama umeimarishwa pindi kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu kitakapoanza rasmi.

Waziri huyo ametoa kauli hio hapa Mombasa kwenye kikao kilichowaleta pamoja maafisa wakuu wa utawala kutoka mikoa yote ya humu nchini pamoja na makamishna wa kaunti zote 47.

Matiang'i amesema kama idara ya usalama wanalo jukumu la kuhakikisha kwamba usalama wa taifa umeimarishwa kikamilifu.

Amewataka maafisa hao kushirikiana na jamii pamoja na taasisi nyingine kufanikisha hali hiyo na kutoruhusu kuchipuka kwa kundi lolote ambalo litaendeleza vitendo ambavyo vinatishia usalama wa kitaifa.

Matiang’I amewaonya dhidi ya kuegemea mirengo ya kisiasa wanapotekeleza majukumu yao nyanjani na kuongeza kwamba hatua hiyo huenda ikalemaza utendakazi wao na kupelekea kudorora kwa usalama.

Aidha Matiang’i amesema idara ya usalama nchini itawawezesha maafisa hao kutekeleza kazi yao kama ipasavyo kikatiba kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha.

Amewataka kutotishwa na mwanasiasa yeyote kabla, wakati na hata baada ya kipindi cha kampeni kuelekea uchguzi mkuu wa Agosti 9.

 Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo