Huku ulimwengu ukiadhimisha uhuru wa vyombo vya habari, shirika la waandishi wa habari la Kenya Correspondent Association limezitaka taasisi za serikali kuhakikisha kuwa uhuru wa wandishi habari umelindwa vyema.
Mwenyekiti wa shirika hilo kanda ya pwani Baya Kitsao amesema kuwa kwa miezi ya hivi karibuni waandishi habari wamekuwa wakipitia madhila mengi mikononi mwa maafisa wa polisi katika eneo la pwani.
Kulingana na Baya visa vingi vya wanahabri kudhulumiwa kikazi viliweza kushuhudiwa hasa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ambapo wanahabari walishambuliwa na maafisa wa polisi wakiwa kazini.
Mwenyekiti huyo pia amekashifu vikali hatua ya wizara ya usalama wa ndani ya kuwakataza wandishi habari kuangazia moja kwa moja mauaji ya halaiki katika eneo la shakahola.
Mwandishi habari Francis Mwaro amewataka wananchi kushirikiana na wandishi habari katika kuendeleza kazi zao badala ya kuwavamia kwa misukumo ya hisia tofauti tofauti.
Kulingana na Mwaro amepitia hali ngumu hasa katika kuangazia mauaji ya halaiki ya shakahola na pia kuangazia matukio katika kanisa la New life church lililoko Mavueni.
Mwandishi habari Triza Auma amewataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha kuwa wamewalipa vizuri wandishi wao.
Kulingana na Triza wanahabari wengi wanapitia masaibu mengi tokea kuanza kwa wimbi la virusi vya Corona.